MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imesema itaanza kusikiliza ushahidi wa upande wa Jamhuri dhidi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), William Mhando, mke wake Eva Mhando, na wenzao watatu, Agosti 26, mwaka huu.

Mhando na wenzake wanakabiliwa na mashitaka sita ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka, kughushi na kujipatia Sh. Milioni 31.7 kwa njia ya udanganyifu.

Kesi ilipangwa kusikilizwa ushahidi huo, Julai 29 na 30, mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi Frank Moshi lakini kutokana maadhimisho ya sikukuu ya Idd, imetajwa na kupangwa tarehe nyingine ya kusikiliza.

Pia,  Mhando anakabiliwa na matumizi mabaya ya madaraka kwa kuipa zabuni Kampuni ya Santa Clara Supplies Ltd, huku akijua ana maslahi nayo na kwamba anaimiliki yeye, mke na watoto wake.

Mbali na Mhando na Eva, washtakiwa wengine ni, France Mchalange, Sophia Misidai na Naftali Kisinga.

Mwendesha Mashitaka wa Taasisi wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai  alidai kuwa kati ya Aprili Mosi na Desemba 31, mwaka 2011 katika ofisi za Makao Makuu ya Tanesco jijini Dar es Salaam, Mhando akiwa mwajiriwa kama Mkurugenzi wa shirika hilo, alitumia vibaya mdaraka yake.

Alidai kuwa, Mhando alitumia vibaya madaraka yake kwa kuamgalia maslahi yake binafsi baada ya kuipa zabuni ya kusambaza vifaa vya ofisi kampuni hiyo inayongozwa na mke wake,  Eva na watoto wake, vyenye thamani ya Sh. Milioni 884.5 na kuisababishia kampuni hiyo kupata faida ya Sh. 31,747,000 kinyume cha sheria .

Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa kati ya Januari 6 na Julai 30, mwaka 2011, mahali pasipofahamika, jijini Dar es Salaam, Eva alighushi taarifa ya ukaguzi wa fedha ya Kampuni ya Santa Clara Ltd,  akionyesha kwamba imekaguliwa na Finx Capital House Desemba mwaka 2010.

Swai alidai katika shitaka la tatu, Agosti 9, mwaka 2011 jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Eva alighushi nyaraka za umiliki wa hisa  kutoka Santa Clara Supplies Ltd kwenda Eveta John Shing’oma huku akijua siyo kweli.

Upande huo wa Jamhuri ulidai katika shitaka la nne, Agosti 5, mwaka 2011 katika ofisi za Makao Makuu ya Tanesco, jijini, mshtakiwa Eva aliwasilisha nyaraka za manunuzi za kughushi akionyesha kwamba taarifa hiyo imeandaliwa na Finx Capital House huku akijua siyo kweli.

Katika shitaka la tano, ilidaiwa kuwa  kati ya Aprili Mosi na Oktoba 31, mwaka 2011 jijini Dar es Salaam,  Eva akiwa kama Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Santa Clara Limited kwa nia ovu, alijipatia faida ya Sh. Milioni 31.7 kutoka Tanesco baada ya kuwasilisha nyaraka za ukaguzi za kughushi.

Ilidaiwa katika shitaka la sita, Oktoba 17, mwaka 2011 katika ofisi za Tanesco, mshtakiwa wa tatu hadi wa tano, Mchalange, Misidai na Kisinga wakiwa watumishi wa shirika hilo, walipokea nyaraka za kughushi na kusababisha Kampuni ya Santa Clara Supplies Limited  kupewa mkataba wa kusambaza vifaa vya ofisini.

Ilidaiwa kuwa mkataba huo ulisababisha kampuni hiyo kupata mkataba wa zabuni ya kusambaza vifaa vya Sh. Milioni 884.5 na kupata faida ya Sh. Milioni 31.5.

Washtakiwa walikana mashitaka hayo kwa nyakati tofauti na wako nje kwa dhamana  hadi Agosti 26, mwaka huu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...