Viongozi na Watumishi wa umma wameaswa kuzingatia Kanuni za Maadili ya utendaji kazi ili kujenga Utawala Bora na kuimarisha mapambano dhidi ya Rushwa nchini.

Rai hiyo imetolewa na Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Mst.) Salome Kaganda wakati akizindua filamu ya “The Minister” iliyoandaliwa na Kampuni ya Equity Links Enterprises (ELE) katika ukumbi wa CENTURY CINEMAX THEATRE Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Kaganda alifafanua kuwa katika utumishi wa umma kuna Kanuni za Maadili ya utendaji zinazowahusu watumishi wenye kushika nyadhifa fulani za uongozi na Kanuni zinazowahusu watumishi wote wa umma. Aidha, Mhe. Kaganda aliendelea kusema kuwa Kanuni hizo zimeainishwa katika Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya 1995, Kanuni za Maadili ya Utumishi wa Umma za 2005 na Kanuni zinazohusu Taasisi za Kitaaluma.

“Mwitikio wa watumishi wa umma kwa Kanuni hizo ni muhimu katika kujenga Utawala Bora yakiwemo mapambano dhidi ya rushwa. Maadili katika utumishi wa umma wa nchi yeyote ni lazima yalenge katika kuainisha misingi ya mwenendo mwema wa mtumishi wa umma kwani misingi hivyo inatarajiwa kukuza dhana nzima ya uwajibikaji na uwazi kwa watumishi wa umma” alifafanua Mhe. Kaganda.

Mhe. Kaganda aliendelea kubainisha kuwa ni wajibu wa mtumishi wa umma kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zinazomwongoza. Aidha, Mhe. Kaganda aliendelea kusisitiza kuwa Mtumishi wa Umma anatakiwa kutekeleza na kusimamia sera na malengo ya serikali kwa juhudi, uaminifu na uadilifu.

Akizungumza kuhusu filamu ya “The Minister” Mhe. Kaganda aliwapongeza waandaaji wa Sinema hiyo na kuelezea hisia zake kuwa filamu hii itasaidia kufundisha na kuwakumbusha Viongozi pamoja na Watumishi wa Umma kuhusu matatizo ya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, uzembe, ubadhirifu na ufuska.
Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Mst.) Salome Kaganda akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa filamu ya “The Minister”, uzinduzi huo ulifanyika katika ukumbi wa Century Cinemax uliopo katika jengo la Dar Es Salaam Free Market, jijini Dar es Salaam.
Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Mst.) Salome Kaganda akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kuzindua filamu ya “The Minister”.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...