Na Mwandishi Maalum, New York 
Wakati Taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ikionyesha ongezeko la watu wanaoishi katika umaskini Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania imetaka utekelezaji wa Malengo Mapya ya Maendelevu Endelevu baada ya 2015 ujielekeze zaidi katika kuukabili umaskini wa vijijini. 
Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, ameyasema hayo siku ya jumatano wakati alipokuwa akichangia majadiliano ya Taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu utekelezaji wa mwongo wa pili wa utokomezaji umaskini ( 2008-2017) 
Katika taarifa hiyo ambayo iliwasilishwa mbele ya Kamati ya Pili ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya Uchumi na Fedha imebainishwa kuwa, licha ya kuwa kidunia idadi ya watu wanaoishi katika umaskini imepungua, idadi ya watu maskini Barani Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara imeongeza kufikia watu milioni 414 kwa takwimu za mwaka 2010. 
 Hata hivyo taarifa hiyo inatoa matumaini ya kwamba idadi hiyo inaweza kupungua na kufika watu milioni 408 ikifikapo mwaka 2015 pale tu jitihada za sasa za kuupunguza umaskini zitakuwa endelevu. 
“ Ninapenda kugusia eneo moja la umaskini, eneo ambalo ninaamini linahitaji umakini katika ajenda za maendeleo endelevu baada ya 2015. Na jambo hili si jingine zaidi ya umaskini wa vijijini.” amesema Balozi Manongi 
Amesema takwimu zinaonyesha kuwa katika kila watu wanne wanaoishi vijijini watatu kati yao wanaishi katika umaskini uliokithiri na kwamba ni wachache sana ambao wameweza kujikwamua na hali hiyo. Balozi Manongi amewaeleza wajumbe wa Kamati hiyo kuwa pale hali ya mambo inapozidi kuwa ngumu, ndipo wananchi hao wanapolazimika kuhamia mijini kutafuta maisha bora, ambayo hata huko mijini hayapo. 
Amebainisha kuwa uhamaji wa watu kutoka vijijini kwenda mijini Kusini mwa Jangwa la Sahara ni moja ya tatizo kubwa linalochangia ongezeko kubwa la idadi ya watu mijini. 
 Akitoa mfano mfazo zaidi wa dhana nzima ya umaskini wa vijijini, Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, amesema hata tatizo la ukataji miti ovyo kwaajili ya kutengeneza mkaa pamoja na matumizi makubwa ya nishati hiyo, ni moja ya kielelezo cha umaskini. 
“ Niruhusuni nibadilishane nanyi uzoefu kuhusu dhima zima ya umaskini hasa umaskini wa vijijini, matumaini yangu ni kuwa pengine itasaidia kutoa picha halisi ya ukubwa wa tatizo la umaskini. Wakazi wengi wa vijijini wanajishughulisha na utengenezaji wa mkaa kama njia ya kujipatia kipato na nishati na matokeo yake ni uharibifu mkubwa wa mazingira ” akasema Balozi. 
 Akaongeza kuwa uharibifu huo wa mazingira kwa maana ya ukataji miti unatokana na mahitaji makubwa ya nishati ya mkaa maeneo ya mijini, nishati ambayo kwa wengi inaoneka kuwa ni ya gharama nafuu.
 “ Majiji na Miji ya Tanzania inatumia tani milioni moja za mkaa kwa mwaka. Asilimia 70 ya matumizi hayo ni katika jiji la Dar es Salaam. Hii ni sawa na upotevu wa ekari 109,500 za misitu.”amesema. 
Balozi Manongi amesisitiza kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea na juhudi zake za kudhibiti matumizi ya nishati hiyo ya mkaa ambayo inaathari kubwa kwa mazingira. Hata hivyo amesema utumiaji mkubwa wa nishati hiyo unatokana na ukweli kwamba anayetengezena anahitaji kipato cha kuendesha maisha yake ili hali anayetumia kwake ni nishati nafuu na anayoihitaji kwa matumizi yake. 
Na kwa sababu hiyo,  Balozi Manongi akasema,   katika mazingira ya namna hiyo, panahitajika mbinu mbadala na ubunifu ambao utakuwa na ufumbuzi endelevu ili kuondokana na umaskini uliokithiri kwa wananchi wengi waishio vijijini. 
Akasisitiza kuwa ajenda ya kuutokomeza umaskini bado ni ajenda muhimu sana kwa mataifa mengi na akasema Tanzania inashukuru kwamba suala hilo limezingatiwa ipasavyo katika matayarisho ya ajenda mpya za maendele. Lakini akaonya kuwa muda wa maneno umekwisha kinachotakiwa sasa ni utekelezaji. 
 Katika hatua nyingine Muwakilishi huyo wa Tanzania, amesema ni jambo lisilo kubalika na hasa kutokana na kiwango kikubwa cha maendeleo katika eneo la utabibu na ubunifu wa tiba kwamba bado watoto chini ya miaka mitano na wanawake wajawazito wanaendelea kupoteza maisha kwa matatizo yatokanayo na umaskini. 
 Vile vile akaongeza kuwa ni jambo pia lisilo kubalika kuwa duniani kote zaidi ya watu bilioni moja hawajui kusoma wala kuandika na huku wengine wakiendelea na utamaduni wa kutokutumia vyoo. “Takwimu hizi zinasikitisha ni wazi kwamba zinahitaji ufumbuzi wa haraka, kila nchi inaowajibu wa kutekeleza, ni lazima basi tutimize wajibu wetu kitaifa na kimataifa. Ahadi zilizotolewa kwa nchi zinazoendelea ikiwa pamoja na zile ambazo ziko nyuma kimaendelea zinatakiwa kutimizwa” amesisitiza Balozi Manongi. 
Taarifa hiyo ya Katibu Mkuu pamoja na kuelezea kwa kina juhudi za kuutokomeza umaskini pia imebainisha sababu zinazopelekea umaskini kuendelea kuwapo. Baadhi ya sababu hizo ni ukosefu wa ajira hususani kwa vijana,pengo kubwa kati ya walio nacho na wasionacho, mabadiliko ya tabia nchi na umaskini na vipaumbe vya kisera
 Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi akizungumza wakati wa kuijadili Taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa  Mataifa  kuhusu utokomezaji wa umaskini. Taarifa hiyo ilijadiliwa  Katika Kamati ya Pili ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.  Kamati hii inahusika na masuala ya Uchumi na Fedha.  Tanzania pamoja na mambo mengine imesisitiza kuwa pamoja na kwamba suala la kutokomeza umaskini  bado ni ajenda muhimu, mkazo  sasa unatakiwa kuelekezwa vijijini ambako bado umaskini ni mkubwa.
Sehemu ya  Wajumbe wa Kamati ya  Uchumi na Fedha ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, wakati wa majadiliano  kuhusu taarifa ya  Katibu Mkuu  ya  utekelezaji wa  mwongo wa kuutokomeza umaskini taarifa hiyo imeainisha  mafanikio na changamoto.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...