Jumamosi   Oktoba 11, 2014 fainali za Miss Tanzania  zilifanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam. Umati mkubwa wa wapenzi wa urembo waliokusanyika hapo ulishuhudia Bi. Sitti Abbas Mtemvu akinyakua taji hilo, akiwashinda warembo wengine 29 na kuwa malikia wa 20 wa urembo nchini.
Sitti, aliyeanza mbio za kuwania taji hilo katika awamu ya vitongoji kwa kujisafishia njia kwa  kuibuka Miss Chang’ombe na baadaye Miss Temeke,  alifuatiwa na  Lillian Kamazima aliyekuwa mshindi wa pili na mshindi wa tatu alikuwa  Jihhan Dimachk.
Kama ilivyo ada, kwenye ushindani pana kushinda na kushindwa. Vile vile penye kushinda ama kushindwa kuna furaha na  kuna manung’uniko, kwa pande husika wa  hayo.  
Kwa ushindi wa Sitti yote hayo yalitokea kwa pamoja kama ilivyokuwa katika fainali kadhaa zilkizopita.
Historia inasema kwamba kila palipofanyika mashindano ya Miss Tanzania, kumekuwepo na aina Fulani ya tafrani. Tokea mashindano ya kwanza yaliyofanyika mwaka 1967,  ambapo mrembo Theresa Shayo (namba 5, picha ya chini) alishinda, mashindano yakapigwa marufuku kwa kuonekana ni kinyume cha maadili ya Mtanzania.
Mwaka 1994 wadau kadhaa wakajitokeza na kufufua mashindano hayo. Bi Aina Maeda akaibuka kuwa mshindi  wa kwanza, wa pili akiwa Lucy Ngongoseke na watatu akawa  Dotto Abuu.  
Zogo likaibuka hapo kuwa  Aina kapendelewa maana hakuwa akiishi nchini, na kwamba aliingia mashindanoni moja kwa moja akitokea Afrika mashariki.
Emily Adolph wa Dodoma alishinda taji hilo mwaka 1995, na zogo lake likawa ameshiriki kinyume na matarajio kwani alikuwa bado ni mwanafunzi.  Mwaka uliofuatia, yaani mwaka 1996, Shose Sinare akateuliwa kuwa Malkia wa Urembo Tanzania. 
Huyu alikuwa na vigezo vyote, ikiwa ni pamoja na sura na umbo zuri na msomi. Tatizo kwake lilikuwa ni kimo. Wadau wakalalamika kuwa hakustahili kuwakilisha nchi kwa kuwa mfupi.
Mambo hayakuishia hapo. Mwaka 1997 mshindi alikuwa Saida Kessy kutoka Arusha,  ambaye hakulalamikiwa sana, kama ilivyokuwa kwa Miss Tanzania wa miaka ya 1998 (Basila Mwanukuzi), 1999 (Hoyce Temu), 2000 (Jaquiline Ntuyabaliwe),  2001 (Happiness Magese), na mwaka 2002 (Angela Damas).
Zogo liliibuka  Mwaka 2003 wakati mrembo Sylvia Bahame alipovaa taji hilo, malalamiko yakiwa kwamba pamoja na kuwa mzuri kwa sura, lakini maumbile yake manene pamoja na meno yenye mwanya vilizua tafrani. Mrembo Faraja Kotta alifuatia mwaka 2004, ambapo hakukuwa na malalamiko sana.
Mwaka 2005 Miss Tanzania Nancy sumari ndiye pekee ambaye alipokelewa vyema na karibu kila mtu, hasa hasa alipoweza kushika nafasi ya tano kwenye mashindano ya dunia. Rekodi ambayo haijavunjwa na yeyote hadi dakika hii. Nancy anaendelea kuwa mfano wa kuigwa hadi leo hii ambapo hana tone la ‘skendo’ ya aina yoyote maishani mwake – kabla na hata baada ya U-Miss. 
Mshindi wa mwaka 2006 alikuwa Wema Sepetu, ambaye kibinfasi hakuwahi kulalamikiwa sana, akafuatiwa na  Richa Adhia mwaka 2007. Huyu alisumbuka sana kutokana na malalamiko kuwa alikuwa ni Mhindi, jambo ambalo wapinga ubaguzi wa rangi waliweza kupigania na kushinda. Ila zogo lake halikuwa dogo…
Nasreen Karim alivaa taji mwaka 2008, na akamaliza muda wake bila zogo, akifuatiwa na Miriam Gerald mwaka 2009, kabla ya Genevive Emmanuel Mpangala kuvaa taji mwaka 2010, na kubahatika kumaliza muda wake bila makelele.  Mwaka 2011 aliibuka Salha Israel, akafuatiwa na Lisa Jensen mwaka , ambaye alimpasia taji Brigit Alfred mwaka 2013. Wote walikuwa hawana matatizo.
Tatizo limeibuka mwaka huu wa 2014 katika umbo la  mshindi wake Sitti Abbas  Mtemvu, ambaye kwa wiki ya pili sasa kila upenyo wa habari umeelezea wasiwasi kuhusu umri wake, na huko mitandaoni nakala za leseni ya udereva na hata hati ya kusafiria vimesambazwa kudai kuwa ana umri wa miaka 25. Wengine walibandika hata picha za mrembo huyo akiwa amebeba mtoto, waliyedai kuwa ni wake – ambavyo ni kinyume cha kanuni za kamati ya Miss Tanzania.
Jana, Kamati ya Miss Tanzania ikiwa chini ya Mwenyekiti wake Anko Hashim Lundenga, pamoja na Miss Tanzania 2014, Sitti Abbas  Mtemvu,  na mama yake mzazi, walikutana na wanahabari kufafanua utata huo wa umri na madai ya kuwa mrembo huyo hana au ana mtoto. Vyote walikanusha na kutoa cheti cha kuzaliwa kinachoonesha kuwa kazaliwa Mei 31, 1991.
Mkutano huo na wanahabari haukuweza kumaliza kiu ya wadau na wadadisi, na badala yake ukawa kama umechochea kuni katika sakata zima la umri wa Sitti. Wengi wakidai kwamba mchanganuo wa umri wake pamoja na masuala ya ,miaka ki- elimu vina wasiwasi, hivyo makelele yanaendelea.
Hatuna nia ya kujiweka upande wowote katika hilo. 
Tahariri hii ina kusudio la kutafuta suluhu katika swala hilo, ili kulinda heshima si ya shindano hilo pekee bali pia jina la Tanzania katika tasnia hiyo na nyinginezo, maana hilo linasambaa hadi kwenye tasnia zote zinazoshirikisha vijana, utamaduni na michezo.
Ushauri wetu ni  kwamba vyombo vyote husika,  chini ya Wizara ya Habari, vijana , utamaduni na michezo, visiache hili liendelee kuwa gumzo mitaani na mitandaoni na kuendelea kuliweka rehani jina la Tanzania Kimataifa. Hatua za makusudi na haraka zichukuliwe ili kieleweke.
Globu ya Jamii inashauri sakata hili lipatiwe muarobaini haraka sana. Iundwe tume huru itayoshirikisha wataalami na wadau wanaohusiana na tasnia hiyo pamoja  vyombo vya  dola na kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli ujulikane. Miss Tanzania ni mwakilishi wa wananchi wote wa Tanzania na si wa kundi la watu fulani.  Hivyo muafaka wa jambo hili unahitajika siku tatu zilizopita.
Endapo ukweli utapatikana na kudhihirika kuwa Miss Tanzania 2014 Sitti Abbasi  Mtemvu hana hatia, basi aombwe radhi kistaarabu nasi sote tujipange nyuma yake na kumsaidia katika maandalizi yake ili akafanye vyema huko kwenye Miss World.
Na endapo atapatikana na hatia, inabidi awajibike yeye mwenyewe kwa kuvua taji hilo. Hapo kamati ya Miss Tanzania nayo itabidi iombe radhi Watanzania kwa kizaazaa hiki. Hili pia liwe kama kengele ya kuamsha, ambapo huko mbeleni yanayojazwa kwenye fumo za washiriki lazima yahakikiwe na wataalamu husika kwa kila jambo.
Wakatabahu

Ankal






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 23 mpaka sasa

  1. Msimtafutie sababu za kumtetea sasa amedanganya umma na ame fake Cheti angekuwa mtu wa kawaida nje kashafungwa.

    ReplyDelete
  2. Nashukuru kwa tahariri nzuri tusiharibu jina letu kwa shida ndogo ndogo ndio kisa umaarufu tu Liangalie hili kwa jicho la pili . TANZANIA nakupenda iwe haina majungu

    ReplyDelete
  3. Ni kweli kabisa. Jambo la kwanza la kwa hiyo tume kuangalia ni kwa nini umri wa mtu unatofautiana kwenye Passport na kwenye Cheti cha Kuzaliwa? La kuongezea katika tahariri hii ni kwamba kuna watu kwenye idara na Passport au kwenye taasisi ya vizazi na vifo (RITA) na wao vile vile waende ma maji baada na kutoka kwa matokeo ya tume hii ambayo nataka iongozwe na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Wadhanini wa Miss Tanzania watoe fedha kufanikisha shughuli za hii tume, la sivyo watakuwa wana support mshindi ambaye anakuwa disqualified kwenye mashindano ya dunia kwa sababu sisi tusiotaka ubabaishaji tutapeleka kwa hao waandaji nakala za Passport na American Driver Licence za mhusika na kucoppy idawa husika za Marekani kuweka wazi utata huu.

    ReplyDelete
  4. MISS WORLD CONTACTS:

    http://www.missworld.com/Contact/

    Twitter: @MissWorldLtd

    ReplyDelete
  5. I would not care less about miss Tanzania.
    Kuna mambo muhimu yanayoendelea hapa duniani kuliko hili.
    Siju watanzania wenzangu mnaelewa jinsi gani huyu kirusi wa EBOLA anavyoenea kwa kasi Africa na duniani.
    Ebola Virus: EBOV is an RNA virus and a member of Filoviridae.

    Fruit bats are the reservoir for EBOV, but outbreaks are due to person-to-person transmission of these viruses, which happens via direct contact with the body, bodily fluid or contamited clothes, utensils (sahani, vijiko, glasi nk.

    Incubation period: siku mbili mpaka wiki tatu!

    Dalili za mwanzo: homa kali, maumivu ya koo, mwili na misuli kuuma, kuumwa kichwa, kuharisha na kutapika.

    Asilimia 30 mpaka 50 ya wagonjwa wanapata dalili za mvujo wa damu (haemorrhagic symptoms),mafigo, ini, mfumo wa fahamu vyote vina athirika na kusababisha "shock" and death.

    Hivyu ndugu zangu, tujiangalie sana, hampa kupeana mikono, usile denda mtu usiyemjua, tule vyakula nyumbani-vyombo vioshwe uzuri,nk.

    Huyu KIRUSI anapatika sana kwenye, damu, matapishi, uharo, na vimaji maji vyote vya mwilini.

    Huyu virus ana usongo, unaweza peana mkono na mgonjwa halafu uka tia kidole chako puani, basi tayari umeshaulamba.
    Dr Gangwe Bitozi.

    ReplyDelete
  6. Asante kwa taarifa zako nzuri
    Sally

    ReplyDelete
  7. PETITION PETITION PETITION...LAZIMA LUNDENGA ALIPE KWA UTAPELI

    ReplyDelete
  8. Hapo umesema kweli Ankal. Tunataka tusiabike kama nchi huko Miss World, ni aibu sana hata michezo inafisadiwa jamani!!! Wapeni walioshinda haki yao, hili la Lundenga kujitokeza na kukomalia ushindi usio wa kweli ni aibu kwake, kwa huyo Sitti na kwa wazazi wake. Kauli alizotoa Lundenga ni potofu eti kuwa wanapeleka majina 12 ya majaji BASATA halafu yachaguliwe 9. Je anachaguaje hayo majina? anatumia kigezo gani? Katika nchi kama yetu iliyojaa rushwa kupindishwa kwa sheria ni jambo jepesi sana, watu hawana professionalism bali wanajali maslahi na kama kuna hongo ndogo tu matokeo huwa yanapindishwa. Tumeona kwenye siasa na wizi wote unaotokea serikalini unafumbiwa macho sembuse miss World. Binafsi sina chuki na huyo aliyeshinda na wala huwa sifuatilii haya mambo ya umiss lakini imenisikitisha kuona wenye uwezo na madaraka wamevuka mipaka hadi kwenye mambo ya wazi wanabadilisha kumsaidia motto wao....HILO HALITAWEZEKANA. Kama mtanzania aishiye hapa USA nitaandika barua miss World (Mr. TRUMP) kueleza hilo na kutoa vithibitisho kuhusu umri na udanganyifu huo ili Tanzania itolewe na kuadhibiwa kwa hilo. HAIWEZEKANI HUO NI UHUNI ULIOKUBUHU,tunaachia vitu vidogo baadaye vinatugharimu kwa sababu hatuna ushujaa wa kusema na tunaishi kwa kuogopeshwa.

    ReplyDelete
  9. Wabongo kweli matatizo unataka iundwe tume ya nini wakati udanganyifu uko wazi. Kwenye maswali masema umri wake miaka 18, leo anasema kazaliwa 1991, vielelezo vingine ambavyo ni nyaraka za serikali ya Tanzania na Marekani vinaonyesha kazaliwa 1989 sasa tume ya nini? Huyu ni wa kufunguliwa mashitaka ya kughushi vyeti na kuudanganya umma

    ReplyDelete
  10. Lundenga hapa jua KANJIBHAI wewe? Mtu kakutoa tongotongo za macho leo unamgeuka? UTAMTAMBUA.

    ReplyDelete
  11. Ivi TAKUKURU mpo hii imekaaje manake kuna viashiria vya ile kitu roho inapenda waziwazi (RITA, UHAMIAJI, KAMATI MISS TZ Kuanzia Kitongojini, Majaji, kwa wazazi, serikali ya mtaa kutaja kwa uchache. Kazi kwenu

    ReplyDelete
  12. Leo Ankal angalau na wewe umetoa mchango wako maana kuna wakati tunajiuliza hivi unakuwa umejiridhisha vipi na habari unazopewa. Kweli tunahitaji mwarobaini maana hii imekuwa kero sasa. Ukilala ukiamka Sitti. Ningekuwa yeye ningeshavua taji lenyewe kung'ang'ania anaonyesha kiburi na desperation wakati anaturingia anasafiri sana. Utadhani watanzania wengine hawasafiri. Shame on this 2014 Miss thing.

    ReplyDelete
  13. Hili suala ni la kipolisi hakuna kuongea,uhamiaji wana taarifa za passport ya siti na vizazi na vifo wanataarifa kwa hiyo kazi wahusika

    ReplyDelete
  14. Binti kaharibu, siku atakapo toa mguu wake nje ya Tanzania nitajua kweli huku nchini hakuna sheria wala haki. Kwakuwa atakuwa amesafiri na hati ya kugushi hivyo maafisa wa uhamiaji mkae macho labda abadili jina. Katutangazia mwenyewe kwamba hati yake ya kusafiria kagushi kwahiyo soo mara mbili, bongo na mamtoni. Liwe fundisho kwetu wote wachakachuaji

















    ReplyDelete
  15. JK alipata tuzo ya utawala bora Afrika sasa kama haya yataachiliwa kwa kusema kuwa mbona wengine wanapeta au kuna mambo muhimu ya kujadili. Sie tunatetea credibility ya JK wetu. Msiiaibishe nchi yetu kesha jenga jina zuri kimataifa.

    ReplyDelete
  16. Dr Gangwe Bitozi, ni kweli hili la Ebola ni tatizo kubwa. Ila na hili la kughushi vyeti (kama ni kweli) nalo pia ni tatizo. Kumbuka habari za ARV feki. Lazima tujifunze kuwa waadilifu katika kila jambo. Kama tutadharau hili la vyeti na pasi feki kesho tukifanyiwa vipimo vya Ebola feki tusilalamike.

    ReplyDelete
  17. tume ya nini kupoteza hela tu wakati kila kitu kinajulikana kuwa kweli amefoji.

    Wapo watu waliosoma wote tokea shule ya vichekechea, shule ya msingi na sekondari kote huko kuna ushaidi tosha.

    Hati yake ya kusafiria tumeona, cheti chake cha kuzaliwa orijino tumekiona(sio kile kipya kwenye press conference) na leseni yake ya kuendeshea gari ya Tanzania pamoja na Marekani (TX) tumeona zinasema miaka tofauti na aliyosema kwenye Miss Tanzania na jana kwenye press conference alivyobadilisha tena mwaka wa kuzaliwa.

    Hili ni swala na intergrity na ethics, viongozi wetu hawana hata uwezo wa kusimamia ukweli kwenye jambo dogo kama hili, je kweli wanaweza kusimamia mikataba ya kuinufaisha nchi hasa mtu wa kawaida aka mlala hoi?

    Hatuwezi kuliachia hili jambo lipite tu kwani huko ni kukubaliana nalo na kutosimamia ukweli. Nchi ijengwe kwenye misingi ya ukweli ndio tutaona taifa lisonga mbele.

    ReplyDelete
  18. Hili liko wazi mnoooo.
    Tusipoteze muda wa kulijadili sana. Vyombo vya DOLA vimeshaliona watalishambulia kama mpira wa kona. TAKUKURU, POKLISI, UHAMIAJI, NK.
    Lazima fundisho lipatikane sasa.

    ReplyDelete
  19. Nakuunga mkono ankal Michuzi...
    Tume huru iundwe kuchunguza hili
    dada alisema hajajiandaa kujibu baadhi ya maswali...sidhani mtu anatakiwa kujiandaa kuelezea uhalisia/facts

    ReplyDelete
  20. mwenye wivu ajinyonge SITI HUYO ANAPAA, NGOMA NZITO HIYO

    ReplyDelete
  21. Nchi hii kama una pesa na madaraka basi kila kitu ni chako. Huyu dada ameshapata nchi hii ndivyo inaenda tutabakia kuandika kwenye mitandao mwenzetu huyo....!!!

    ReplyDelete
  22. hiyo ndo Tanzania.

    ReplyDelete
  23. Nchi imeharibiwa na viongozi wa kwanza waliolazimisha umaskini. Watu wakaangukia kuwa walafi. Neema ingeruhusiwa naturally raia wangeona utajiri na kupata kuwa ni vitu vya kawaida. Kinyume chake tulibanwa mno na sasa tumeangukia katika kuabudu rushwa, uongo, choyo, wivu na kutotosheka. Mfano halisi wa Tanzania ya leo ni mtoto aliyewekewa 'geti kali'. Siku akipata mwanya anakuwa hakamatiki.
    Kwa mtazamo wa kawaida huyu Siti anawakilisha jamii nzima. Watu kama hawa wako kila pembe ya nchi. Kudanganya na kughushi imekuwa dili otherwise mafanikio hayaji. Wengi tumepitia huko na haya ni majuto kwani majuto ni mjukuu huja baada ya kitendo. Kitendo cha utawala wa kwanza kutufungia geti kali matokeo yake sasa hatukamatiki tena na tusimnyooshee kidole huyu binti tu kwani hili ni janga letu sote.
    Mndengereko Ukerwe

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...