Timu ya Taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ imeondoka saa 9.45 alfajiri ya leo Juni 30, 2016 kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia kwenda Visiwa va Hame-Shelisheli kwa ajili ya kuwavaa wenyeji katika mchezo wa marudiano kuwania nafasi ya kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana.

Serengeti Boys inaondoka na matumaini makubwa ya kuiondoa Shelisheli katika mbio hizo baada ya kuvuna ushindi mnono wa mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Jumapili ya Juni 26, 2016. Ili ifuzu, Serengeti Boys inahitaji kusimama imara katika matokeo hayo ama kwa kupata sare ya aina yoyote, kushinda au ikitokea kupoteza, basi isifungwe zaidi ya mabao 2-0.

Lakini Kocha Mkuu wa vijana hao, Bakari Shime maarufu kama Mchawi Mweusi kutoka Tanga, amesema, “Nawaheshimu Shelisheli, lakini vijana wangu hawawezi kuwapa nafasi hata kidogo wapinzani wetu. Hapa tulishinda, na kwako tunakokwenda tunakwenda kushinda. Vijana wangu wa Serengeti Boys wako vizuri. Nawapenda na wao wanatupenda makocha wao na viongozi wote wa TFF.”
Katika mchezo wa Dar es Salaam waliozifumania nyavu walikuwa Nickson Kibabage, Ibrahim Abdallah na Ally Hussein ambaye alifunga ambao kila mmoja amepania kufunga kama kocha akiwapa nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza kwa sababu Mchawi Mweusi amefunga safari hiyo akiwa na kikosi cha nyota 20 wa timu hiyo inayolelewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) chini ya Rais Jamal Malinzi.

Nyota waliosafiri ni pamoja na makipa, Ramadhani Awm Kabwili na Samwel Edward Brazio wakati mabeki wako Kibwana Ally Shomari, Nickson Clement Kibabage, Israel Patrick Mwenda, Dickson Nickson Job, Ally Hussein Msengi, Issa Abdi Makamba.

Viungo ni Kelvin Nashon Naftal, Ally Hamisi Ng’anzi, Asadi Ali Juma Ali, Syprian Benedictor Mtesigwa, Ibrahim Abdallah Ali, Yassin Muhidini Mohamed, Shaban Zuberi Ada huku washambuliaji wakiwa ni Rashid Mohammed Chambo, Mohammed Abdallah Rashid, Yohana Oscar Mkomola, Muhsin Malima Makame na Enrick Vitalis Nkosi.

Serengeti Boys ambayo haina mdhamini badala yake ikihudumiwa na TFF yenyewe ilikuwa kambini tangu Juni 14, 2016 kujiandaa na mechi hizo za kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Shelisheli na Afrika Kusini ambayo itapambana nayo baadaye mwezi ujao.

Katika kuajindaa na mchezo huo, Serengeti Boys ilifanya ziara India ambako walishiriki mashindano ya vijana ya Kimataifa yanayotambuliwa na FIFA (AIFF International Youth Tournament 2016) kabla ya kurudi na rekodi ya kupigiwa mfano si tu katika Tanzania na kwa nchi za Afrika Mashariki. Ilishika nafasi ya tutu nyuma ya Korea Kusini na Marekani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...