Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Katika jitihada zake za kuongeza ufanisi na huduma bora, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limefungua ofisi za kanda katika mikoa ya Arusha, Mwanza na Mbeya.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Dkt. Egid Mubofu (pichani) amewaambia waandishi wa habari jana jijini hapa kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa bidhaa zinazozalishwa au kuuzwa kwa watanzania zinakuwa na ubora na viwango vinavyotakiwa.

“Ofisi hizi zitafanya kazi kwa karibu na wazalishaji viwandani ili wananchi wapate bidhaa bora,” alisema na kuongeza kuwa watendaji katika ofisi hizo watakuwa wanafanya ukaguzi  viwandani na kushughulika na maombi ya wazalishaji wapya.

Alisema ofisi ya mkoa wa Arusha itahudumia mikoa ya kanda ya kaskazini ikiwemo Manyara, Kilimanjaro, Tanga na Arusha yenyewe; Ofisi ya Mwanza itahudumia Kanda ya ziwa mikoa ya Mara, Kagera, Shinyanga, Simiyu, Geita na Mwanza yenyewe.

Ofisi ya Mbeya itahudumia mikoa ya nyanda za juu Kusini ya Iringa, Songwe, Ruvuma, Njombe na Mbeya yenyewe.

Dkt. Mubofu alisema kwa muda mrefu wazalishaji wa bidhaa viwandani walikuwa wakipata huduma makao makuu ya shirika Dar es Salaam na hivyo kusababisha ucheleweshaji wa huduma.

Alisema ofisi hizo zitafichua viwanda bubu vinavyo zalisha bila kufuata utaratibu.

“Ilikuwa ni vigumu kwa shirika kugundua uwepo wa viwanda bubu katika maeneo ya mikoani na wilayani kwa urahisi kutokana na umbali lakini sasa kazi itafanyika bila kikwazo,”alisema.

Pia shirika limefungua ofisi mipakani katika mipaka ya Mutukula, Kasumulo na Tunduma.  Awali ilisha fungua ofisi Holili, Horohoro, Sirari, Namanga na Rusumo.

Alisema kwa upande wa bandari wamefungua ofisi katika bandari ya Mwanza na Mombasa na pia wamefungua ofisi katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

“Ufunguzi wa ofisi za mipakani unalengo la kupunguza miaya ya uingizaji holela wa bidhaa hafifu katika soko la Tanzania unaofanywa na wafanyabiashara wasio waaminifu,” alisisitiza Dkt. Mabofu.

Akitoa mfano alisema ufunguzi wa ofisi katika bandari ya Mwanza na Mombasa utapunguza uingizaji bidhaa hafifu toka nchi jirani za Kenya na Uganda.

Alisema shirika limejipanga vyema na kuwataka wananchi kushirikiana na ofisi za mamlaka nchini kufichua viwanda vinavyozalisha na wafanyabiashara wanaokiuka utaratibu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...