Imebainika kuwa Bandari ya Zanzibar ni miongoni mwa Vyanzo vya Mapato vinavyopelekea ukuaji wa uchumi baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na fursa zilizopo katika nyanza za biashara. 
Hayo yamebainishwa leo na Mkurugenzi Mkuu wa Bandari ya Zanzibar Captain Abdallah Juma Abdallah katika siku ya pili ya ziara ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba ambapo amepata fursa ya kutembelea Bandari ya Zanzibar.
Katika siku ya pili ya ziara yake ya siku saba Visiwani Zanzibar Waziri Makamba amebainisha kuwa lengo la ziara yake ni pamoja na kufuatilia utekelezaji wa masuala waliyokubaliana katika vikao baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar katika vikao vya mashirikiano.
"Niko Zanzibar kwa ziara ya kikazi na nimejikita zaidi katika kushughukikia masuala ya uchumi ikiwa ni pamoja na masuala ya Bandari, Forodha, Kodi na kubaini changamoto zilipo, utekezaji wa maazimio yaliyokubaliwa katika vikao vya majadiliano na kuangalia maeneo mapya yanayohitaji kuingizwa katika mfumo wa utatuzi," Makamba alisisitiza.
Waziri Makamba amesema kuwa kuwepo kwa bandari ni ufanisi kwa uchumi na ni namna bora ya kuimarisha  Muungano  na ustawi wa Zanzibar na pande zote mbili za Muungano hazina budi kuondoa changamoto zilizopo kwa manufaa ya wote.
Waziri Makamba pia amepata fursa ya kutembelea Mamlaka ya Mapato Tanzania na Bodi ya Mapato Zanzibar na kuwafahamisha kuwa lengo la Serikali zote mbili ni kuhakikisha kuwa pande zote mbili za Muungano zinanufaika na fursa za uchumi zilizopo, na kila upande unufaike na fursa zilizopo katika mambo ya Muungano na yale yasiyo ya Muungano.
Katika ziara hiyo Waziri Makamba amewataka  watendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania upande wa Zanzibar kuzifanyia kazi changamoto ndogo ndogo zinazojitokeza kwa haraka, kupunguza urasimu na kuongeza elimu kwa umma ili kujenga uelewa kwa wananchi  juu ya mambo yanayopaswa kuzingatiwa na yale yasiyopasa ili kuondoa vikwazo vinavyojitokeza katika bandari ili kuondoa malalamiko ya wananchi.
Nae Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania  kwa upande wa Zanzibar Bw. Mcha Hassan Mcha amesema kuwa ni vema wananchi wazingitae kanuni, taratibu na miongozo iliyopo ikiwa pamoja na kupata risiti halali kwa kila bidhaa wanazonunua ili kuepuka usumbufu pindi wasafirishapo bidhaa baina ya Tanzania bara na Zanzibar. 
Ziara ya Waziri Makamba visiwani Zanzibar itaendelea kesho kwa kutembelea miradi mbalimbali ya Mazingira.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais  Muungano na Mazingira Mhe January Makamba (kushoto) akimsikiliza Kapteni Abdallah Juma Abdallah Mkurugenzi Mkuu wa Bandari - Zanzibar alipokuwa akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa kazi za bandari mara baada ya Waziri Makamba kupata fursa ya kuwatembelea.
 Viongozi waandamizi wa Bandari - Zanzibar wakifafanua jambo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais  Muungano na Mazingira Mhe January Makamba alipotembelea bandari hiyo hii leo kujionea utendaji kazi wao na kuwapa fursa ya kuianisha changamoto zinazowakabili na kuweka mikakati ya kukabiliana nazo.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais  Muungano na Mazingira Mhe January Makamba (katikati) akifafanua jambo kwa Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar  wa (pili kulia). Waziri Makamba amefanya ziara ya kutembelea ofisi zao na kupata fursa ya kufanya majadiliano kwa manufaa na ustawi wa Muungano wetu. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais  Muungano na Mazingira Mhe January Makamba akiwa katika kikao na Menejimenti ya Bodi ya Mapato Zanzibar. Wa pili kushoto ni Kamishna wa Bodi Bw. Amour Hamil Bakari na Bi. Khadija Shamte  Naibu Kamishna. Waziri Makamba yuko ziarani Zanzibar kutembelea Taasisi za Muungano na zile zisizo za Muungano.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...